Chanjo yatumainiwa miezi miwili ijayo
Sisti Herman
May 26, 2026
Share :

Chanjo ya majaribio ugonjwa wa Ebola inayotengenezwa na watafiti waliohusika na chanjo ya Uviko-19, inatarajiwa kuanza ndani ya miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa.
Tayari majaribio ya chanjo hiyo kwa wanyama yameanza ikiwa ni juhudi za kukabiliana na kuenea kwa ugonjwa huo.
Mkuu wa Kitengo cha Kinga katika Taasisi ya Sayansi ya Magonjwa ya Mlipuko ya Chuo Kikuu cha Oxford, Teresa Lambe amesema wanatumia teknolojia sawa na waliyotumia kutengeneza chanjo ya Uviko-19 kutengeneza chanjo ya kirusi cha Ebola aina ya Bundibugyo.
Kupitia video hiyo iliyochapishwa na Shirika la Habari la Uingereza la Reuters, Lambe amesema kwa kawaida utengenezaji wa chanjo na majaribio huchukua miaka mitano hadi 10 kukamilika.
Amesema sasa kinachofanyika ni juhudi za haraka kutafuta chanjo ya virusi hivyo.
“Kama mambo yatakwenda kama tulivyotarajia, tunategemea majaribio ya chanjo yataanza ndani ya miezi miwili hadi mitatu kuanzia sasa,” amesema.





