China yawahukumu kifo mawaziri 2, kisa rushwa
Eric Buyanza
May 8, 2026
Share :

Mahakama ya kijeshi nchini China imewahukumu kifo mawaziri wawili wa zamani wa ulinzi baada ya kupatikana na hatia ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
Hukumu hiyo ilitangazwa Alhamisi kupitia vyombo vya habari vya serikali ya China.
Mawaziri hao ni Wei Fenghe na Li Shangfu, ambao walifikishwa katika mahakama ya kijeshi na kuhukumiwa kifo huku adhabu hiyo ikisitishwa kwa miaka miwili.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Xinhua, baada ya kipindi hicho hukumu zao zitabadilishwa kuwa kifungo cha maisha bila nafasi ya msamaha au kupunguziwa adhabu.
Mahakama ilisema viongozi hao walipokea kiasi kikubwa cha rushwa na kutumia nyadhifa zao kujinufaisha binafsi pamoja na kuwapa wengine upendeleo usio halali. Mali zote binafsi za wawili hao pia zimechukuliwa na serikali.
Li Shangfu alikuwa Waziri wa Ulinzi kuanzia Machi 2023 kabla ya kuondolewa madarakani Oktoba mwaka huo baada ya kutoweka hadharani kwa muda mfupi. Naye Wei Fenghe alihudumu katika nafasi hiyo kuanzia 2018 hadi 2023 kabla ya kurithiwa na Li.
Hukumu hizo zinatajwa kuwa sehemu ya kampeni kubwa ya kupambana na rushwa inayoendeshwa na Rais Xi Jinping ndani ya jeshi na serikali ya China. Hata hivyo, wakosoaji wa serikali wanasema kampeni hiyo pia hutumika kuwaondoa wapinzani wa kisiasa wa rais huyo.
BBC





