Clara Luvanga avunja rekodi ya usajili wa soka la wanawake duniani?
Eric Buyanza
September 11, 2026
Share :

Mshambuliaji wa Tanzania Clara Luvanga amejiunga na Washington Spirit akitokea klabu ya Saudi Arabia, Al-Nassr, katika usajili unaoaminika kuwa miongoni mwa usajili wenye gharama kubwa zaidi katika historia ya soka la wanawake.
Ada iliyolipwa na klabu hiyo ya Ligi ya Marekani kwa wanawake (National Women's Soccer League) haijawekwa wazi rasmi.
Baadhi ya taarifa zinaripoti kuwa ni dola milioni 2.3 (takriban pauni milioni 1.7), jambo ambalo lingemfanya Luvanga kuwa mchezaji wa kike aliyesajiliwa kwa gharama kubwa zaidi katika historia ya soka la wanawake.
BBC haijaweza kuthibitisha kiasi hicho, ingawa chanzo kilicho karibu na suala hilo kimesema kinaamini usajili huo unaingia katika orodha ya usajili ghali zaidi wa soka la wanawake, ukiwa miongoni mwa sajili tano bora na ghali.
Spirit ilikataa kusema kuhusu ada hiyo ya uhamisho ilipowasiliana na BBC Sport.
Luvanga, mwenye umri wa miaka 21, amesaini mkataba utakaomuweka Washington hadi mwisho wa msimu wa 2029 wa NWSL.
Iwapo kiasi hicho cha rekodi kilichoripotiwa ni sahihi, itamaanisha ada hiyo imevuka pauni milioni 1.4 ambazo London City Lionesses inadaiwa kuilipa Paris St-Germain kumsajili Grace Geyoro mwaka jana.
Hata hivyo, ada ya Geyoro imepingwa, jambo linaloonyesha zaidi jinsi takwimu za uhamisho katika soka la wanawake mara nyingi zinavyofanywa kuwa siri.
Kwa uhamisho huo, pia Luvanga anakuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza katika moja ya ligi kubwa za wanawake duniani ya NWSL.
Luvanga alitwaa taji la ligi kuu la Saudi Arabia kwa wanawake( Saudi Women's Premier League) katika misimu yake yote mitatu akiwa na Al-Nassr, pamoja na Saudi Women's Cup, Saudi Women's Super Cup na Mashindano ya Klabu za Wanawake ya West Asian Football Federation (WAFF).
Pia alitwaa kiatu cha dhahabu cha ligi msimu uliopita baada ya kufunga mabao 24 katika mechi 14.
Washington Spirit inamilikiwa na Michele Kang, ambaye pia anaimiliki London City Lionesses.





