Coutinho na utepe mwekundu wa bahati aliopewa na Messi
Eric Buyanza
May 20, 2026
Share :

Hapo awali utepe huo mwekundu wa kuvaa mkononi ulikuwa ukimilikiwa na mama wa mwandishi wa habari wa Argentina Rama Pantarotto. Wakati wa Kombe la Dunia la mwaka 2018, mama huyo alimwomba mwanae (Rama) ampe Messi utepe huo na auvae kwa ajili ya kumuongezea bahati kwenye michuano hiyo.
Messi alishukuru sana kwa zawadi hiyo, lakini baadae aliamua kumkabidhi mchezaji mwenzake ambaye alikuwa akipitia wakati mgumu.
Mnamo Januari 2019 kabla ya mkondo wa pili wa robo fainali ya Copa del Rey dhidi ya Sevilla, Coutinho alikuwa akipambana kutokana na kushuka kwa kiwango chake.
Messi katika hali ya kutaka kumuongezea ari mchezaji huyo, alimkabidhi utepe huo kama zawadi.
Cha kushangaza ni kwamba, utepe huo ulifanya kazi kwani Coutinho alifunga mara mbili usiku huo na FC Barcelona ilishinda 6-1.
Tangu kipindi hicho Coutinho (kiungo wa kati wa Brazil) amekuwa akiutunza kwa uangalifu utepe huo mwekundu kama ishara ya bahati, lakini pia kama ukumbusho muhimu aliopewa na Messi.





