pmbet

Daktari Bingwa wa kwanza wa mfumo wa chakula na ini kwa watoto

Sisti Herman

May 28, 2026
Share :

 

Tanzania imeandika historia mpya katika sekta ya afya baada ya Dkt. Livin Peter Mumburi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufanikiwa kuwa daktari bingwa wa magonjwa wa mfumo wa chakula na ini kwa watoto, baada ya kuhitimu mafunzo maalum nchini Afrika Kusini.

Dkt. Mumburi anakuwa daktari wa kwanza na pekee nchini Tanzania mwenye utaalamu huo, baada ya kukamilisha mafunzo ya uzamivu wa kimatibabu ya miaka miwili katika Chuo Kikuu cha Cape Town, hatua inayotajwa kufungua ukurasa mpya wa huduma za kibingwa za mfumo wa chakula na ini kwa watoto hapa nchini.

Akizungumza baada ya kurejea nchini, Dkt. Mumburi ameeleza kuwa changamoto za magonjwa ya ini na mfumo wa chakula kwa watoto bado ni kubwa Tanzania, huku akisisitiza kuwa watoto wengi wanahitaji huduma za kibingwa zinazopatikana kwa uchache.

“Changamoto za magonjwa ya ini na mfumo wa chakula kwa watoto ni kubwa sana Tanzania. Watoto wengi wanahitaji huduma za kibingwa ambazo hapo awali zilikuwa chache sana. Tunataka kuboresha huduma hizi hapa nchini ili watoto wapate matibabu bora bila kulazimika kwenda nje ya Tanzania,” amesema Dkt. Mumburi.

Kwa sasa, Dkt. Mumburi anatarajiwa kuimarisha zaidi huduma za mfumo wa chakula kwa watoto Muhimbili kupitia kliniki zilizopo, sambamba na kuharakisha mpango wa kuanzisha kliniki maalum ya ini kwa watoto, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kibingwa nchini na kupunguza utegemezi wa matibabu nje ya nchi.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet