Dangote na utajiri wote bado anaishi kwenye nyumba ya kupanga
Eric Buyanza
July 16, 2024
Share :
Tajiri namba moja barani Afrika, Aliko Dangote amewashangaza wengi baada ya kusema hana nyumba nchi nyingine yoyote zaidi ya Nigeria, jambo ambalo limezua mjadala mkubwa kwenye mitandao ya kijamii....wengi wakisema hiyo sio tabia iliyozoeleka kwa matajiri wa kiafrika.
Tajiri huyo anasema ana nyumba mbili katika mji aliozaliwa wa Kano, na nyingine jijini Lagos na anaishi katika nyumba ya kupanga kila anapotembelea mji mkuu, Abuja.
Dangote aliorodheshwa na jarida la Forbes mwezi Januari kama mtu tajiri zaidi barani Afrika kwa mwaka wa 13 mfululizo licha ya matatizo ya kiuchumi yanayoikumba nchi yake.
Utajiri wake ulipanda kwa $400m zaidi mwaka jana, na kumpa thamani ya jumla ya $13.9bn (£10.7bn), Forbes walisema wakati huo.
Mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 66 alijitajirisha kwa saruji na sukari - na mwaka jana alifungua kiwanda cha kusafisha mafuta jijini Lagos.
"Sababu ya kutokuwa na nyumba London au Marekani ni kuwa nilitaka kuangazia ukuaji wa viwanda nchini Nigeria,".
"Nina shauku kubwa juu ya ndoto ya Nigeria na kando na nyumba yangu ya Lagos, nina nyumba nyingine katika jimbo langu la Kano, na nyingine ya kukodi huko Abuja.
"Ikiwa nitakuwa na nyumba kote Marekani na kwingineko, singeweza kutuliza akili na kufanya kitu kwa ajili ya watu wangu." alisema Damgote.
Matajiri wengine wa kiafrika wanamiliki majumba kwenye miji mikubwa duniani kama vile London, Dubai, Washington na Paris.