Danilo huenda akawa mchezaji wa kwanza kusajiliwa Man United na Amorim
Eric Buyanza
November 9, 2024
Share :
Bosi mpya wa Man Utd, Ruben Amorim anajiandaa kumsajili beki wa zamani wa Man City, Danilo kutoka Juventus, kulingana na ripoti kutoka nchini Italia.
Amorim atachukua rasmi usukani wa kuinoa Man United Novemba 11 mara tu atakapomaliza kusimamia mechi yake ya mwisho ya Sporting Lisbon dhidi ya Braga wikiendi hii.
Tayari wachezaji wengi wamehusishwa kuhamia Man United kipindi hiki ambacho Amorim atakuwa akiumiza kichwa ni namna gani ataweza kuboresha kikosi chake katika dirisha dogo la usajili.
Mshambuliaji wa Sporting Lisbon, Vicktor Gyokeres alikuwa mmoja wa wachezaji wa kwanza waliotengeneza vichwa vya habari kwa tetesi kwamba anaelekea Man United.
Na sasa tovuti ya Kiitaliano ya Juve Live, imeihusisha Man Utd na beki wa kulia wa Juventus, Danilo, ambaye aliwahi kuwachezea mahasimu wa Mashetani Wekundu Manchester City.
Danilo ambaye ni nahodha wa Juventus na Brazil inaonekana yuko karibu kuondoka Italy na taarifa zinadodosa kuwa Amorim anamtaka Man Utd katika dirisha lijalo la usajili.