Dar kukabiliwa na upungufu wa Maji kwa siku 4
Sisti Herman
November 2, 2026
Share :

Wakazi wa maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam wanatarajiwa kukabiliwa na upungufu wa huduma ya maji kwa siku nne kuanzia kesho Jumanne, Novemba 3 hadi 6, 2026, wakati Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) ikifanya matengenezo ya bomba kuu lenye kipenyo cha inchi 72 linalopokea maji kutoka Mtambo wa Ruvu Chini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Dawasa, Everlasting Lyaro, matengenezo hayo ni sehemu ya maandalizi ya kuimarisha miundombinu ya majisafi ili kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El Nino.
Kutokana na matengenezo hayo, uzalishaji wa maji katika mtambo huo utapungua kwa asilimia 60 kwa kipindi cha saa 96, hali inayotarajiwa kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wakazi wanaohudumiwa kupitia chanzo hicho.
Maeneo yatakayoathirika ni pamoja na Zinga, Kiromo, Dunda, Kisutu, Magomeni, Nianjema, Fukayosi, Makurunge, Kerege, Mapinga, Mbweni, Mabopwepande, Bunju, Kunduchi, Kawe, Mbezi Juu, Goba, Wazo, Makongo, Kijitonyama, Kinondoni, Makumbusho, Msasani, Mzimuni, Tandale, Ndugumbi, Kigogo, Kariakoo, Mchikichini, Upanga Magharibi, Gerezani, Upanga Mashariki, Mchafukoge, Jangwani, Kivukoni, Ilala, Mnyamani, Liwiti, Kilungule, Kilakala, Mianzini, Keko, Kurasini, Miburani na Chang’ombe.
Dawasa imewaomba wateja na wananchi katika maeneo hayo kuvumilia usumbufu unaoweza kujitokeza wakati wa matengenezo hayo. Pia, imewahimiza kupanga matumizi ya maji na kuhifadhi kiasi cha kutosha kwa matumizi muhimu kabla ya kazi kuanza ili kupunguza athari za upungufu wa huduma katika kipindi hicho.





