De Bruyne awafuata Kante na Benzema Saudia
Sisti Herman
July 8, 2024
Share :
Kiungo wa Manchester City, Kevin de Bruyne, 33, amefikia makubaliano binafsi kwa njia ya mazungumzo na timu ya Al Ittihad ya Saudi Arabia ambayo anaweza kujiunga nayo katika dirisha hili la usajili linaloendelea duniani.
Kwa sasa matajiri hao wa Kiarabu wanazungumza na Manchester City kumalizana juu ya bei na mchakato mzima wa kumsajili fundi huyo wa kimataifa wa Ubelgiji aliyekuwa akiiwakilisha nchi yake katika mashindano ya Euro 2024 walikotolewa hivi karibuni.
Inaelezwa kwamba Man City inataka walau kiasi kisichopungua Pauni 100 milioni kutoka kwa matajiri hao na ikiwa itashindikana inaweza kumuuza kwa mkwanja usipungua Pauni 70 milioni.
Inadaiwa kwamba Al Ittihad imemwandalia nyota huyo mshahara wa Pauni 1.1 milioni kwa wiki ambao utakuwa mara tatu zaidi ya ule anaoupokea kwa sasa kutoka kwa matajiri wa Jiji la Manchester.
Mkataba wa De Bruyne unamalizika 2025, ambapo wababe wa Etihad wapo tayari kumuuza kwa sababu wakikomaa naye kikosini hadi dirisha lijalo la majira ya kiangazi atakuwa na uwezo wa kuondoka bure na isipate chochote. Mchezaji huyo alikuwa na msimu mzuri uliopita licha ya awali kuwa majeruhi.