Declan Rice atajwa miongoni mwa wachezaji hatari wa Uingereza.
Joyce Shedrack
July 15, 2026
Share :
Wakati mashabiki wakiwasifu nyota wa Uingereza Jude Bellingham na Harry Kane, gazeti la Clarin la nchini Argentina limemtaja kiungo Declan Rice kuwa mchezaji ambaye mabingwa watetezi Argentina wanapaswa kumdhibiti kwa umakini mkubwa.

"Rice ndiye nguzo ya uwiano wa timu. Anawalinda mabeki wa kati, anaziba nafasi mabeki wa pembeni wanapopanda kushambulia, na pia huiongoza timu katika kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma."
Mbali na Declan Rice, gazeti la Clarin pia limemtaja Elliot Anderson kuwa mmoja wa wachezaji muhimu ambao Argentina inapaswa kuwadhibiti katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Uingereza.
"Anderson ndiye kiungo kinachounganisha sehemu zote za timu. Hujitengenezea nafasi ya kupokea mpira, huupokea, hugeuka na kuendelea kujitafutia nafasi nyingine ya kuucheza."
Clarin liliongeza kuwa vita vya eneo la kiungo vitakuwa muhimu katika mchezo huo, likisisitiza kuwa kocha wa Argentina, Lionel Scaloni, atalazimika kuweka presha si kwa mabeki wa kati wa Uingereza pekee, bali pia kwa Rice na Anderson.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, lengo kuu litakuwa kuwazuia viungo hao kupokea mpira wakiwa wanaelekea mbele, jambo ambalo linaweza kuvuruga mfumo wa England wa kuanzisha mashambulizi na kuongeza nafasi ya Argentina kufuzu fainali ya pili mfululizo ya Kombe la Dunia.





