Dereva afia kwenye gari baada ya kuwasha jiko la mkaa ili kuota moto
Eric Buyanza
July 27, 2024
Share :
Thadei Mbawala, mkazi wa Mtaa wa Mjimwema, Halmashauri ya Mji Njombe, mkoani hapa, amefariki dunia ndani ya gari baada ya kuwasha mkaa ili kuota moto na kupitiwa na usingizi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi (ACP) Mahamoud Banga, alithibitisha jana kutokea kwa tukio hilo juzi majira ya saa moja asubuhi ambapo pembeni ya mwili huo kulikutwa jiko la mkaa lililowashwa.
Alisema dereva huyo alikuwa kwenye gari lenye namba za usajili T 983 BZZ aina ya Fuso, mali ya kampuni ya maji ya Kitulo.
“Chanzo cha tukio hili ni dereva huyo Julai 24, mwaka huu, usiku kuingia kwenye gari akiwa na jiko la mkaa na wakati anachaji simu yake alipitiwa na usingizi na kufariki dunia kwa sababu ya kuvuta hewa ya sumu ya mkaa.
“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Njombe kuacha tabia ya kutumia majiko ya mkaa wakiwa wamejifungia ndani kwa kuwa ni hatari kwa afya zao,” alionya Kamanda Banga.