Dereva wa gari la Chadema akamatwa kwa kusababisha ajali
Sisti Herman
June 6, 2025
Share :
Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limemkamata dereva Yahaya Bakari Idd (43) mkazi wa Gongo la Mboto Mkoa wa Dar es salaam baada kusababisha ajali iliyotokea Juni 5, 2025 katika eneo la Mataa ya Tumbaku kata ya Mafisa Manispaa ya Morogoro.
Taarifa ya leo Juni 6, 2025 iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama imeeleza kwamba dereva huyo amesababisha ajali hiyo akiwa anaendesha gari namba T.661 DQL aina ya Ford Ranger mali ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa uzembe wa kutozingatia alama za barabarani na kusababisha gari hilo kuacha njia na kuligonga gari jingine T.340 DWW/T.976 CJE aina ya Scania ambalo lilikuwa limeegeshwa kwenye kisima cha Mafuta.
Kufuatia ajali hiyo abiria watatu waliokuwa kwenye gari hilo wamepata michubuko na majeraha madogo ambapo wametibiwa na kuruhusiwa huku jeshi la Polisi likiendelea kuwashauri madereva kuheshimu alama za barabarani ili kujiepusha na matukio ya ajali.