Dickson, kijana wa miaka 25 aoa Bibi wa miaka 70
Eric Buyanza
July 9, 2024
Share :
Katika hali ya kushangaza, kijana wa miaka 25 kutoka kitongoji cha Murehwa huko nchini Zimbabwe ameiacha jamii inayomzunguka ikiwa na mshangao baada ya kutangaza hadharani mapenzi yake kwa bibi kikongwe cha miaka 70.
Licha ya kukabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa familia ya mwanaume, lakini wawili hao ni kama wameweka pamba masikioni na kuliendeleza penzi lao.
Chanzo kinaeleza kuwa kijana huyo aliyetambulika kwa jina la Dickson, ana historia ya mahusiano yasiyo ya kawaida.
Hapo awali, alimpeleka kumtambulisha kwao mwanamke mzee ili amuoe lakini hakukubaliwa na mama yake, hali iliyoleta sintofahamu kiasi cha Dickson kufukuzwa kwenye nyumba ya familia.
Sasa safari hii kijana Dickson amekuja na kali nyingine kwa kuingia kwenye mahusiano na Bibi kizee wa miaka 70 ambaye ana watoto saba na wajukuu chungu tele.
Hata hivyo mahusiano hayo yamepingwa vikali na Baba mzazi wa Dickson huku akitishia kutumia nguvu kuliharibu penzi la wawili hao.
Kwa kujibu hilo, Dickson ametishia kuikana familia yake na kuanza maisha mapya na mpenzi wake huyo.
Uhusiano huo sio tu umesababisha ugomvi ndani ya familia ya Dickson pekee, bali hata kwenye familia ya bibi huyo ambapo watoto wake wanahisi kuaibishwa, na wamediriki hata kumshambulia Dickson.
Wakuu wa kijiji cha Murehwa wamejaribu kuvunja mahusiano hayo bila mafanikio, badala yake, hali hiyo imezidisha dhamira ya Dickson ya kubaki na mpenzi wake, na hata kuapa kufa kwa ajili yake.