DKT.Samia atoa wito "Vunjeni makundi tusiishiwe pawa kama wale".
Joyce Shedrack
September 6, 2025
Share :
Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa wanachama wa chama hicho mkoani Iringa kuvunja makundi yaliyoundwa wakati wa mchakato wa uteuzi wa wagombea na kuungana kwa mshikamano kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Akizungumza Jumamosi Septemba 06, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mafinga, Dkt. Samia amesema mchakato wa uteuzi umemalizika na wagombea waliopitishwa sasa wanapaswa kuungwa mkono na kila mwanachama wa CCM bila kujali tofauti zilizokuwepo awali.
“Uteuzi wa wagombea umekamilika ndani ya CCM, ninatambua wakati wa kugombea makundi yalikuwa mengi sana, wagombea walikuwa wengi sana. Lakini tumemaliza uteuzi, ninataka kuwaambia WanaMafinga, walioteuliwa ndiyo Mungu aliwawekea mkono, ambaye hakuteuliwa subiri wakati mwingine. Niwaombe sana sana tuvunje makundi… ili twende kwenye uchaguzi tukiwa wamoja, chama kikiwa na nguvu, tusiishiwe ‘pawa’ kama walivyoishiwa wenzetu,” amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia amesisitiza kuwa mshikamano wa chama ni silaha muhimu ya ushindi, hivyo kila mwanachama anatakiwa kuweka mbele maslahi ya chama na si maslahi binafsi.