Dr. Alinda Mashiku, Mtanzania anayeongoza wanaanga NASA
Sisti Herman
April 15, 2026
Share :

Dr. Alinda Mashiku ni mhandisi mbobezi kutoka Tanzania anayeng’ara kimataifa katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM). Kwa sasa anafanya kazi katika Kituo cha teknolojia ya anga za juu cha NASA (National Aeronautics and Space Administration) cha Goddard Space Flight Center (GSFC) nchini Marekani, mojawapo ya vituo muhimu vinavyoongoza utafiti na maendeleo ya anga za juu.
Ameweka alama ya kipekee kwa kuwa sehemu ya timu ya misheni ya Artemis II, hatua muhimu katika safari ya kurejesha binadamu Mwezini baada ya zaidi ya miaka 50 tangu enzi za Apollo.
Katika mradi huo, Dr. Alinda anahudumu kama Deputy Mission Systems Engineer akihusika na mifumo ya mawasiliano na urambazaji wa anga (Exploration and Space Communications).
Jukumu lake linahakikisha kuwa chombo cha anga kinaweza kuwasiliana na Dunia na kujua kwa usahihi kilipo na kinakoelekea, mambo ambayo ni msingi wa usalama na mafanikio ya safari hiyo.
Alizaliwa Marekani na kukulia Tanzania kabla ya kwenda tena Marekani kwa masomo ya juu. Alipata shahada ya kwanza katika Uhandisi wa Mitambo (Mechanical Engineering), na baadaye shahada ya uzamivu (PhD) katika Uhandisi wa Anga na Anga za Juu (Aerospace Engineering) kutoka Chuo Kikuu cha Purdue. Elimu hii ilimjengea msingi imara uliomwezesha kushiriki katika miradi mikubwa ya anga.
Ndani ya NASA, amejikita katika urambazaji wa vyombo vya anga, uchambuzi wa mizunguko (orbit analysis), pamoja na uongozi wa kiufundi katika timu za wahandisi. Uwezo wake wa kuunganisha taaluma na uongozi umechangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya misheni za kisasa za anga.
Zaidi ya taaluma, Dr. Alinda ni chanzo kikubwa cha msukumo kwa vijana wa Kitanzania na Afrika, hususan wasichana. Ameendelea kusisitiza kuwa ndoto kubwa zinawezekana, bila kujali unapotoka.





