EBOLA: Kenya yatangaza kifo cha pili
Eric Buyanza
October 24, 2026
Share :

Kenya imethibitisha kifo cha pili cha Ebola. Mwanamke mwenye umri wa miaka 65 aliyefariki alikuwa ndugu wa karibu wa mgonjwa wa kwanza, na alianza kuonyesha dalili akiwa karantini jijini Nairobi.
Kenya imethibitisha kifo cha pili kutokana na ugonjwa wa Ebola, huku mamlaka za afya zikisema hakuna ushahidi wa maambukizi kusambaa katika jamii nje ya kundi la watu waliokuwa na uhusiano na mgonjwa wa kwanza.
Wizara ya Afya ilisema Ijumaa, Oktoba 23, kuwa aliyefariki ni mwanamke mwenye umri wa miaka 65, aliyekuwa ndugu wa karibu wa Mkenya aliyefariki kutokana na ugonjwa huo mapema mwezi huu. Mwanamke huyo alikuwa miongoni mwa watu waliowekwa karantini baada ya kuwa karibu na mgonjwa wa kwanza.
Alianza kuonyesha dalili siku kumi kabla ya kifo chake na kulazwa katika kitengo cha magonjwa ya kuambukiza jijini Nairobi, ambako alipatiwa huduma za kupunguza makali ya ugonjwa na kusaidia mwili kupambana nao.
Wizara ilisema wahudumu wa afya walifanya kila lililowezekana kuokoa maisha yake, lakini alifariki Ijumaa jioni. Familia yake imejulishwa na mipango ya mazishi salama yenye kuheshimu utu wa marehemu itaandaliwa kwa kushirikiana na ndugu zake.
Wagonjwa wengine saba wanaendelea kutibiwa katika vituo viwili vya kutengwa. Kwa jumla, Kenya imethibitisha maambukizi tisa, yakiwemo ya watu wawili waliofariki. Hakuna maambukizi mapya yaliyotangazwa katika taarifa hiyo.
DW





