Ebola yatua mji wa Bukavu unaodhibitiwa na waasi wa M23
Eric Buyanza
May 22, 2026
Share :

Kundi la waasi la M23 limesema kisa cha kwanza cha Ebola kimethibitishwa katika jimbo la Kivu Kusini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, eneo lililo chini ya udhibiti wake.
Kwa mujibu wa msemaji wa M23, mgonjwa huyo mwenye umri wa miaka 28 alitokea mjini Kisangani, lakini alifariki dunia kabla ya majibu ya vipimo kuthibitisha kuwa alikuwa ameambukizwa Ebola. Kisa hicho kimerekodiwa mjini Bukavu, mji mkuu wa Kivu Kusini uliotekwa na M23 mwaka jana.
Mlipuko huo wa Ebola, ambao Shirika la Afya Duniani WHO limeutangaza kuwa dharura ya afya ya kimataifa, unaendelea kuenea huku juhudi za kuudhibiti zikikwamishwa na migogoro ya muda mrefu mashariki mwa Kongo.
Wakazi wa eneo hilo tayari walielezea wasiwasi hata kabla ya kuthibitishwa kwa kisa hicho cha kwanza na hasa kutokana na hali hiyo ngumu iliyochewa na machafuko, kama anavyosema Murhula Machumbiko, “Tunakabiliwa na mgogoro wa kiuchumi na kifedha. Hata kupata sabuni imekuwa tatizo. Tunafikiri kwamba ugonjwa ukiingia hapa, tutashuhudia vifo. Kama unavyojua, jiji la Bukavu lina watu wengi sana.”
Kwa mujibu wa WHO, mlipuko wa sasa ni wa 17 nchini Kongo na tayari vifo 139 vinahusishwa na ugonjwa huo, huku karibu visa 600 vikitiliwa shaka. Serikali ya Kongo bado haijatoa tamko rasmi kuhusu kisa hicho kipya.
DW





