Fadhili atupwa jela maisha kwa kunajisi mtoto wa kike wa miaka minne
Eric Buyanza
May 7, 2024
Share :
Fadhili Shaibu (36), mkazi wa kijiji cha Chiwale wilayani Masasi, mkoani Mtwara amehukumiwa kifungo cha maisha jela baada ya kukutwa na hatia ya kumnajisi mtoto wa kike wa kaka yake mwenye umri wa miaka minne, baada ya kumrubuni kuwa atampa machungwa.
Hukumu hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki mjini Masasi na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Masasi, Batista Kashusha, baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote na kujiridhisha na vielelezo vya ushahidi vilivyotolewa mahakamani na upande wa Jamhuri pamoja na upande wa mashtaka.
Akisoma hukumu hiyo, Kashusha alisema kuwa kesi hiyo namba 93 ya mwaka 2023 ilikuwa na mashahidi watano, na kwamba mahakama imemtia hatiani mshtakiwa kwa kumhukumu kifungo cha maisha jela baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.
Ilidaiwa mahakamani humo kuwa mshtakiwa alifanya kosa la kumnajisi mtoto wa kaka yake Agosti 25, mwaka 2023 majira ya saa 9:30 jioni wakati akiwa nyumbani kwake katika Kijiji cha Chiwale, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi na kumsababishia maumivu makali na kumharibu sehemu za siri.