Familia yahifadhi viungo vya marehemu nyumbani
Eric Buyanza
May 15, 2026
Share :

Familia ya marehemu Thomas Silayo, mkazi wa Tarakea Motamburu wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, imelazimika kuhifadhi baadhi ya viungo vya mwili wa marehemu nyumbani baada ya kujeruhiwa vibaya katika tukio la mauaji linalodaiwa kusababishwa na mgogoro wa ardhi.
Mke wa marehemu amesema mumewe alijeruhiwa vibaya kwa kukatwa na mapanga na mtu anayedaiwa kuwa ndugu yake, hali iliyosababisha kupelekwa katika Hospitali ya Karume kwa matibabu ya dharura.
Amesema kutokana na ukubwa wa majeraha hayo, madaktari walilazimika kuondoa mkono na mguu wa marehemu ili kuokoa maisha yake kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC kwa matibabu zaidi.
“Walivitoa viungo na kuviweka pembeni, kisha wakaviweka kwenye mfuko wakati tukielekea KCMC kwa ajili ya matibabu zaidi,” amesema mke wa marehemu.
Aidha, amesema walipofika KCMC waliomba viungo hivyo vihifadhiwe hospitalini lakini walishauriwa kuvihifadhi wenyewe wakati matibabu yakiendelea.
Marehemu Thomas Silayo alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu kutokana na majeraha aliyoyapata katika tukio hilo.
Mke huyo amesema alirejea nyumbani akiwa amebeba mkono na mguu wa mumewe katika mifuko maalum iliyowekwa na askari kuzuia damu kuvuja, hali iliyowaacha ndugu na majirani wakiwa katika taharuki kubwa.
Amesema alipofungua mmoja wa mifuko hiyo mbele ya baadhi ya watu waliokuwepo nyumbani, wengi walikimbia kwa hofu baada ya kushuhudia sehemu za mwili wa marehemu.
“Nilifungua ule mfuko watu wakaanza kukimbia kwa hofu, ilikuwa hali ya kuogopesha sana,” amesema.
Kwa mujibu wa maelezo yake, hali ya mumewe hospitalini ilikuwa mbaya kiasi cha kuwatia hofu hata ndugu waliokuwa wakifika kumuona kutokana na majeraha makubwa aliyokuwa nayo.
Tukio hilo limewaacha wananchi wa Rombo wakiwa na mshtuko mkubwa huku wengi wakitaka uchunguzi wa kina kufanyika kuhusu tukio hilo linalodaiwa kuhusishwa na mgogoro wa kifamilia uliodumu kwa muda mrefu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linaendelea kumtafuta mtuhumiwa wa tukio hilo lililotokea Mei 8, 2026 wakati familia ikijiandaa kufanya kikao cha kutatua mgogoro wa mipaka ya shamba uliodumu kwa zaidi ya miaka 30.
HABARILEO





