FIFA hatarini kumnyang’anya Trump tuzo ya amani
Eric Buyanza
October 17, 2026
Share :

Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limeanzisha rasmi mchakato wa kutathmini upya na kupitia mustakabali wa tuzo yake ya amani (FIFA Peace Prize), ambayo kwa mara ya kwanza na ya pekee ilitolewa kwa Rais wa Marekani, Donald Trump.
Hatua hiyo imekuja kufuatia kikao cha Baraza la FIFA kilichofanyika tarehe 15 Oktoba 2026 jijini Zurich, Uswisi, ambapo uamuzi ulifikiwa wa kukabidhi suala hilo kwa Kamati ya FIFA ya Wajibu wa Kijamii katika Soka ili ifanye uchunguzi wa kina.
Tuzo hiyo iliundwa kwa ghafla na Rais wa FIFA, Gianni Infantino, mnamo Novemba 2025 na kukabidhiwa kwa Trump mwezi mmoja baadaye (Desemba 2025) wakati wa hafla ya droo ya Kombe la Dunia iliyofanyika mjini Washington.
Tangu wakati huo, uamuzi huo umekuwa ukikosolewa vikali na wadau wa soka duniani pamoja na baadhi ya wajumbe wa bodi ya FIFA. Wakosoaji wanahoji kuwa kutoa tuzo hiyo kwa kiongozi wa kisiasa ni ukiukwaji wa wazi wa kanuni kuu za FIFA zinazotaka chombo hicho kutojihusisha kabisa na masuala ya kisiasa.
Baraza la FIFA linachunguza jinsi tuzo aliyopewa Donald Trump ilivyoundwa na kuamuliwa. Kutokana na uchunguzi huo, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea kwa mambo mawili......kufutwa kabisa kwa tuzo hiyo ili kumaliza mzozo au kubadilishwa kwa sheria ili kuzuia wanasiasa kupewa tuzo hiyo baadaye, na badala yake iwe inatolewa kwa watu wanaoleteana amani kupitia soka pekee.
Ripoti na mapendekezo ya kamati hiyo yanatarajiwa kuwasilishwa rasmi katika kikao kijacho cha Baraza la FIFA. Uamuzi wa mwisho kuhusu kama Trump atanyang'anywa tuzo hiyo au kama itafutwa kabisa unatarajiwa kutolewa Desemba 16, 2026, kwenye mkutano utakaofanyika Doha, Qatar.





