FIFA Yakanusha tuhuma za kuiependelea Argentina Kombe la Dunia 2026.
Joyce Shedrack
July 10, 2026
Share :
Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limekanusha vikali madai kwamba waamuzi wake wanaegemea upande wa Argentina katika Kombe la Dunia 2026, likisisitiza kuwa maamuzi ya waamuzi hufanywa kwa uhuru na bila kushawishiwa na mtu yeyote.
Mkuu wa waamuzi wa FIFA, Pierluigi Collina, amesema hakuna msingi wa madai hayo na kusisitiza kuwa hata Rais wa FIFA, Gianni Infantino, hana mamlaka ya kuingilia maamuzi ya waamuzi.
"Hakuna mtu anayeweza kudai kwamba waamuzi wa FIFA wanaweza kushawishiwa na yeyote, hata na Rais wa FIFA, Gianni Infantino. ameendelea kuonyesha imani kamili kwa kikosi cha waamuzi na kuturuhusu kufanya kazi kwa uhuru kamili," alisema Collina.
Aliongeza kuwa waamuzi, kama ilivyo kwa wachezaji na makocha, hufanya kazi kwa uaminifu na kujitahidi kutoa maamuzi sahihi kila wakati.
Kauli hiyo imekuja baada ya kocha mkuu wa Misri, Hossam Hassan, kuibua tuhuma kufuatia timu yake kutolewa na Argentina katika hatua ya 16 bora ya mashindano hayo.
Hassan alilalamikia bao la Misri lililokataliwa pamoja na penalti aliyodai ilistahili kutolewa katika dakika za mwisho wa mchezo, kabla ya Argentina kufunga bao la ushindi pia alidai kuwa mwamuzi wa mchezo huo, Francois Letexier, alikuwa chini ya shinikizo na kueleza kuwa matokeo hayo hayakuwa ya haki.
Hata hivyo, FIFA imesisitiza kuwa tuhuma zisizo na ushahidi hazina nafasi katika mchezo wa soka na kwamba mfumo wake wa uamuzi unaendelea kuzingatia misingi ya haki, uwazi na uhuru wa waamuzi.





