Gachagua; Maisha yangu yapo hatarini
Sisti Herman
April 16, 2025
Share :
Aliyekuwa makamu wa rais wa Kenya, Rigathi Gachagua amemwandikia barua Mkuu wa Polisi nchini humo (IGP), Douglas Kanja akilalamika kuwepo majaribio kadhaa ya kumuua, huku mamlaka nchini humo zikishindwa kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
Katika barua hiyo aliyoichapisha kwenye akaunti yake ya Mtandao wa X leo Jumanne Aprili 15, 2025, Gachagua ametaja majaribio kadhaa yaliyolenga kuondoa uhai wake, familia yake, watu wake wa karibu na uharibifu wa mali zake.
“Kama unavyofahamu, una jukumu la kikatiba la kulinda maisha na mali ya kila Mkenya kama ilivyoainishwa katika katiba ya Kenya ya mwaka 2010. Hata hivyo, katika hali hii, Kanja (IGP) unaendeleza uhalifu na ukatili kwa makusudi,” ameandika Gachagua.
Huku akitaja Kifungu cha 245 cha Katiba ya Kenya, hasa 245(2)(b) Gachagua amesema ni wajibu wa Jeshi la Polisi nchini humo kulinda usalama raia na mali zao, jambo ambalo anadai IGP huyo halitekelezi badala yake anaukingia kifua uovu unaotendwa na Serikali iliyoko madarakani.
Gachagua alipoteza baadhi ya ulinzi wake baada ya kuondolewa madarakani kama Naibu rais wa Kenya kupitia kura ya kutokuwa na imani naye iliyopigwa Oktoba 8, 2024.
Katika siku za karibuni, msafara wa Gachagua ulivamiwa na makundi yanayodaiwa kuwa ni ya vijana wahuni, ambao pia walifanya uharibifu mkubwa wa mali.