Gakpo afunga akiwa na majonzi ya kupoteza mtoto
Eric Buyanza
June 30, 2026
Share :

Mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uholanzi, Cody Gakpo, alionekana akitokwa na machozi baada ya kuifungia timu yake bao katika mchezo wa hatua ya 32 bora dhidi ya Morocco, siku chache baada ya yeye na mpenzi wake kupoteza mtoto wao wa kiume ambaye walikuwa wanatarajiwa kumkaribisha duniani mwezi Oktoba (alikuwa bado hajazaliwa).
Gakpo, mwenye umri wa miaka 27, aliipa Uholanzi bao la kuongoza katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1 baada ya muda wa kawaida na wa nyongeza.
Hata hivyo, Uholanzi iliondolewa kwenye mashindano baada ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti 3-2.
Habari za msiba huo zilitangazwa Jumamosi na mpenzi wake, mwanamitindo Noa van der Bij. Wawili hao walikuwa wanatarajia kumpata mtoto wao wa pili mwezi Oktoba, kabla ya ujauzito huo kuharibika.
Licha ya kipindi hicho kigumu kwa familia yake, Gakpo aliamua kubaki kambini na kuendelea kuitumikia timu ya taifa.
Baada ya kufunga bao, mshambuliaji huyo alipiga magoti huku akionekana kushindwa kuzuia hisia zake.
Wachezaji wenzake walimzunguka na kumfariji, huku nahodha wa Uholanzi na Liverpool, Virgil van Dijk, akimkumbatia walipokuwa wakirejea katikati ya uwanja.





