Gari la mwenyekiti labebwa na mafuriko akiwa anashuhudia
Eric Buyanza
April 12, 2024
Share :
Mvua iliyonyesha kwa masaa saba katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, imesababisha maafa makubwa ya mafuriko yaliyosomba magari, vyakula, vyombo vya ndani, kuharibu mashamba huku ikiacha baadhi ya familia zikikosa makazi.
Tukio lingine ni la kusombwa na maji gari la Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji.
Akiongea na chanzo chetu Mwenyekiti huyo wa Serikali ya Kijiji cha Engorora eneo la Kisongo Mkoani Arusha, Bwana Justine Joel, amesema gari lake lenye namba za usajili T 134 DFK, aina ya Toyota IST ilisombwa na mafuriko aliyokutana nayo njia panda, akitoka ofisini kwake kurudi nyumbani.
"Niikuwa naendesha tulipovuka eneo la ofisi ya kijiji, ghafla nilikutana na maji mengi, ambayo sijawahi kuyaona eneo hili tangu nizaliwe, ambayo yalisababisha gari langu kuzima," amesema.
Amesema milango iligoma kufunguka, hali iliyowalazimu kutokea madirishani na gari hilo likabebwa na mafuriko akiwa anashuhudia kwa macho yake.