Gesi ilipiwe kama Luku, 90% ya Wanzania wanatumia kuni na Mkaa
Sisti Herman
May 8, 2024
Share :
Rais Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Nishati kutafuta Watanzania Wabunifu wa teknolojia na kuwapa kazi ya kufanikisha mpango wa kuwawezesha Watumiaji wa gesi ya kupikia wawe wanalipia kadri wanavyotumia kama inavyofanyika kwenye LUKU za umeme.
Akiongea leo wakati akiuzindua Mkakati wa Taifa wa nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024 Jijini Dar es salaam, Rais Sami amenukuliwa akisema yafuatayo “Serikali tunalo jukumu la kuongeza uelewa kwa Wananchi kuhusu nishati safi ya kupikia na kutunga sera nzuri na wezeshi ili kufikia malengo ya mkakati huu, katika hili wenzetu wa Wizara ya Nishati watatuongoza kuhakikisha nishati safi ya kupikia inapatikana kwa uhakika na kwa bei inayohimilika kwa Wananchi”
“Sekta binafsi tunaitarajia pamoja na kuongeza uwekezaji na kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia sehemu mbalimbali Nchini watuletee pia teknolojia rahisi itakayowezesha Wananchi kupata nishati safi kadri ya uwezo wao kwa mfano kulipia kadri anavyotumia kama inavyofanyika kwa umeme na maji, zile pre paid meters”
“Na hapa nataka niseme Waziri kwamba moja kati ya maonesho ya mazingira niliyowahi kutembelea nishaikuta hii teknolojia kuna Watanzania wametengeneza mitungi ambayo unatumia gesi jinsi unavyolipa, unachukua mtungi mzima kama umelipa elfu 10 utatumia gesi yako ya elfu 10 ikimalizika mtungi unakata hata kama gesi ipo mpaka uwasiliano nao tena ulipe tena wakufungulie utumie tena naomba sana watafute au kama wapo wajitokeze tufanye nao kazi katika eneo hili”
"Mwezi Novemba 2022 tulikuwa na mjadala wa kitaifa wa kuhamasisha uhamiaji kutoka tunavyopika sasa kwenda kwenye nishati safi ya kupikia, pamoja na mambo mengine nilielekeza uandaliwe mkakati wa kitaifa wa matumizi ya nishati safi, nilifanya hivyo kwa sababu maalum kwanza kutokana na ukubwa wa tatizo kwani asilimia 90 ya kaya nchini zinatumia kuni na mkaa," - Rais Samia.
Rais Samia ameyasema hayo leo kwenye hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam tarehe 08 Mei, 2024.