Guardiola alivyokuna upara kwa Build-up za De Zerbi kimbinu
Sisti Herman
May 27, 2024
Share :
Utangulizi
Mara baada ya kutamatika kwa ligi kuu Uingereza msimu wa 2023/24 kocha wa klabu ya Brighton Roberto De Zerbi ametangaza kuondoka kwenye timu hiyo huku akiwa ameacha alama kubwa kwenye timu hiyo na ligi kwa ujumla Kutokana na utambulisho wa mbinu zake.
Kocha huyo hivi sasa anahusishwa na timu kubwa mbalimbali kwaajili ya kujiunga nazo kutokana na vilabu hivyo kuvutiwa na mbinu zake akiwa Broghton na hata kabla.
Mbinu zipi zimemtambulisha De Zerbi?
🗣️ “Brighton chini ya Roberto De Zerbi ndiyo timu inayovutia kwenye ujenzi wa mashambulizi kuanzia nyuma kwenye lango lao”
- Pep Guardiola
Nukuu hii ya Pep Guardiola inatufungulia mjadala kuhusu mbinu za De Zerbi ambaye aliipa Brighton utambulisho wa kuvutia kwa mbinu bora za ujenzi wa shambulizi kuanzia nyuma kwenye lango lao kwa pasi fupi za haraka, fasaha (Build up from back) ambazo ziliwasaidia kwa mara ya kwanza kwenye historia yao kufuzu na kucheza michuano ya Ulaya baada ya kufanya vyema msimu wa 2022/23, kwenye Makala haya tutautumia zaidi msimu huo kuelekea mbinu zake.
Muundo wa timu wakati wa Build up ulikuwaje?
De Zerbi alitumia mfumo wa 4-2-3-1 ambao wakati wa Build up ulinyumbulika kuwa kwenye miundo tofauti kama;
1. Theluthi ya kwanza ya uwanja wakimhusha kipa 3-4-4
Mstari wa kwanza wa ujenzi wa mashambulizi huwa na watu watatu, kipa Sanchez na mabeki wawili wa kati, Webster na Dunk
- Hawa huhusika kwenye ujenzi wa mashambulizi kuanzia kwenye theluthi ya kwanza ya uwanja, kwenye muundo wa watu watatu au -3- kwenye 3-4-4 (Build up phase)
Mstari unaofuata huwa na watu wanne, viungo wawili wa kati Caecedo & MacAllister pamoja na mabeki wa pembeni, Estupina kushoto & Gross kulia
- Hawa huhusika kwenye uendelezaji wa mashambulizi, kwa njia mbili, kati na pembeni kulingana na presha ya wapinzani ili kuuvusha na kufika kwenye theluthi ya pili ya uwanja (Progression)
Mstari wa mwisho huwa na viungo washambuliaji wa pembeni wawili, Mitoma kulia & March kushoto na washambuliaji wa kati Welbeck na Incisio
- Hawa huhusika na kupenya, kutengeneza nafasi na kufunga ambapo viungo washambuliaji wawili wa pembeni hutanua pembeni zaidi, washambuliaji wa kati hugawana, mmoja hushuka katikati ya mistari na mwingine hushambulia nyuma ya mistari ya wazuiaji au wakati mwingine husogea katikati ya msitari wote wawili ili kuwavuta wapinzani na kuacha nafasi kubwa nyuma yao itakayoshambuliwa na viungo wa pembeni (Penetration, Creation and Finishing)
Mistari miwili ya mwanzo, yenye wachezaji 6 (7 na kipa) huwa karibu zaidi na goli lao, kwaajili ya kujenga na kuendeleza shambulizi (Build up and progression) huku Mstari wa mwisho wenye watu wanne, mawinga na washambuliaji ukibaki mbele zaidi ili kuwalazimisha mabeki wa timu pinzani kuendelea kubaki nyuma (pinning back) na Kutengeneza nafasi kubwa Katikati ya mistari
2. Theluthi ya kati na ya mwisho bila kumhusiaha kipa 2-4-4
Wakiwa kwenye theluthi mbili za mbele, yaani ya Kati na ya mwisho hawamhusishi kipa wao kwenye build up zao
Lengo la Brighton kufanya Build up kuanzia nyuma ni lipi?
Lengo kuu la Brighton kujenga mashambulizi kuanzia nyuma ni kuwavuta wapinzani kwa kuwashawishi kushinikiza kuanzia kwao ili kutengeneza kina kikubwa cha uzuiaji kwenye kuta zao za uzuiaji ambacho kitatengeneza nafasi katikati ya mistari au nyuma ya ukuta wao kisha kutumia faida tatu kuwafikia, ambazo ni;
(i) Idadi - Faida ya idadi kwenye kila mstari dhidi ya wapinzani, wao wakifaidika zaidi na uwepo wa kipa kwenye mstari wa Kwanza (Numerical Superiority)
mfano: kama wapinzani wakizuia na muundo wa 4-4-2, wao huwa na faida kwenye mstari wao wa kwanza wa uzuiaji wenye watu watatu dhidi ya ule wa wapinzani wenye watu wawili (3v2)
(ii) Ubora - Faida ya uwezo Kutokana na uwezo wa kiufundi wa wachezaji wa kupiga pasi na kukukokota kwenye nafasi (Qualitative Superiority)
(iii) Nafasi - Faida ya nafasi za kuwafika kwenye lango la wapinzani kirahisi kwa kutumia njia za zinazotokana na nafasi za wazi katikati ya mistari au nyuma ya mstari wa mabeki baada ya kuwavuta kwao (Positional Superiority)
Njia kuu za Build up za Brighton ni zipi?
1. Njia ya kati (Passing Through The Press)
Brighton hupenda kuwatumia viungo wawili wa kati Caecedo na MacAllister (double pivot) kama njia ya kwanza ya kupokea na kuendeleza shambulizi linalojengwa na kipa na mabeki kuanzia nyuma kwa kipa na mabeki wawili, hasa pindi wapinzani wanapozua na stili ya mtu dhidi ya mtu (Man Marking) ambayo huruhusu mianya katikati ya mistari yao ya uzuiaji (build up progressions)
2. Njia ya pembeni (Passing Around The Press)
Pindi njia ya kati inapokuwa imezuiwa vizuri kwa wapinzani ku-press na nidhamu nzuri ya kufinya uwanja na kuwakaba mtu na mtu na nafasi (Zonal Marking) kwa Viungo hao wawili wa kati, Brighton hupenda kuendeleza mashambulizi kwa kutumia mabeki wa pembeni, Gross na Estupina
3. Njia ya juu - (Passing Over The Press)
Wapinzani wanapokuwa wamezuia njia mbili muhimu za Brighton kuendeleza mashambulizi, kwa kuzuia kwa idadi kubwa na kubana uwanja vyema, Brighton hutumia njia za juu kwa pasi ndefu kutoka nyuma, ambapo washambuliaji wao wawili, Welbeck na Incisio husogea hadi Katikati ya mistari ya uzuiaji ya wapinzani ili kuwavuta mabeki wa kati wa wapinzani na kutengeneza nafasi nyuma yao ambayo hushambuliwa na viungo washambuliaji wa pembeni, Mitoma na March
Mambo muhimu kwenye Build up za De Zerbi ni yapi?
1. Pressure Attraction - kama ilivyo kwa Lengo lake la kujenga mashambulizi kuanzia nyuma, Lengo la kwanza la De Zerbi ni kuwashawishi wapinzani kuwafuata ili kutengeneza nafasi kuwafikia kirahisi
2. Superiority - Baada ya kuwashawishi wapinzani kuwafuata, ni ngumu kutoka kwenye Pressure na kuvunja mistari yao ya uzuiaji bila kuwazidi kwa idadi, ubora, hivyo De Zerbi kwenye kila eneo mpira ulipo huhakikisha wachezaji wake wapo kwa idadi kubwa na kutumia ubora wao wa kiufundi ipasavyo kama kupiga pasi sahihi na kukokota kwenye nafasi za wazi
3. Third Man runner - Baada ya kuwa wengi kwenye eneo dogo lenye mpira, De Zerbi hutumia mtu wa tatu kuutoa mpira kwenye pressure, kwani huamini mchezaji wake mwenye mpira na wale waliokaribu kupokea mpira huwa kwenye shinikizo kubwa la wapinzani hivyo huhimiza wakati wachezaji hao hupasiana (mwenye mpira na anayetegemea kupokea) kuwepo na mchezaji wa tatu ambaye anakuwa kwenye nafasi ya wazi nyuma wapinzani ili kuwa tayari kupokea pasi kutoka kwa anayepewa na kuutoa mpira kwenye pressure na kuvunja mistari wa wapinzani
4. Vertical Movement - Pindi wachezaji wanapopasiana, kama nilivyoeleza juu, Mwenye mpira, anayetarajia kuupokea na Yule wa tatu anayetegemea kupokea (third man runner), wachezaji hao wote mikimbio yao na mpira ni lazima iwe inaelekea kwenye lango la wapinzani ili kuweza Kutengeneza nafasi za kufunga
5. Versatility - De Zerbi kwenye mbinu zake huamini kwa wachezaji kubadilishana nafasi uwanjani hasa pale wanapokaribisha pressure kwao, mchezaji wa nafasi moja huweza kuhama na kushambulia nafasi ya wazi kwenye shimo lolote kulingana na namna wapinzani wanavyozuia, hivyo huamini zaidi kwa wachezaji kuwa na uwezo wa kiufundi wa kucheza nafasi tofauti uwanjani (viraka) ndiyo maana amekuwa alibadili miundo na Kikosi na nafasi mara kwa mara, Kikosi nilichotumia pale juu hakijacheza zaidi ya mechi 10 wote kwa pamoja, ina maana wachezaji walikuwa wakibadilishwa mara kwa mara
Athari zinazowakumba kulingana na mbinu zao ni zipi?
1. Quality - Brighton ni timu yenye wastani mzuri wa umiliki wa mpira, utengenezaji wa nafasi lakini wamekuwa wahanga wa kuruhusu magoli mengi kwasababu ya mbinu zao Kukosa wachezaji wa daraja la juu, wanacheza aina ya mpira ambayo kama haina wachezaji wa daraja la dunia kuziwasilisha basi watakuwa wanapokonywa mpira kwenye pressure na kushambuliwa
2. Rest defence - Brighton imeruhusu mabao mengi Kutokana na udhaifu wa kimuundo, wachezaji wao wanapokuwa na mpira hutanua Sana uwanja na kuacha muundo wa nyuma pindi wanapokuwa kwenye nusu ya wapinzani kuwa na idadi ndogo ya wachezaji wenye mabeki wawili wa kati na viungo wawili, hivyo kwenye mashambulizi ya kujibu huwepo kwa idadi ndogo