Haikuwa haki kusimamisha mchezo kama ule - Sadio Mane
Eric Buyanza
January 19, 2026
Share :

Mshambuliaji wa Senegal, Sadio Mane alitumia jitihada kubwa kuhakikisha wachezaji wenzake wanarudi uwanjani kuendelea na mchezo wao dhidi ya Morocco wakati wa fainali ya AFCON usiku wa jana kuamkia leo.
Hilo lilijiri baada ya mchezo huo kusimama kwa muda kuelekea mwisho wa kipindi cha pili baada ya mwamuzi kuwapa Morroco penalti ya dakika za lala salama kufuatia Brahim Diaz kufanyiwa madhambi kwenye eneo hatari, kitendo kilichosababisha kocha wa Senegal na wachezaji wake kutoka nje ya uwanja wakilalamikia uamuzi huo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, kwanini aliamua kuwaita wachezaji wenzake kurudi uwanjani Mane alisema:
“Walipoamua kutoka nje na kutocheza, nilibaki na kuwauliza baadhi yao mnaonaje kuhusu hili, mnadhani ni wazo zuri?'”
"Kisha niliamua kwenda kuwarudisha uwanjani...nadhani lilikuwa jambo bora zaidi kufanya, kwa sababu huu ni mpira tu.....mwamuzi wakati mwingine anaweza kufanya makosa na wakati mwingine akafanya vyema....watu duniani wao ndio wataamua kama ilikuwa penalti ama la, lakini cha muhimu zaidi ilikuwa ni ulimwengu kutazama soka...na haikuwa haki kusimamisha mchezo kama huu" anasema Sadio Mane ambaye hii itakuwa AFCON yake ya mwisho.





