Haitakuwa haki mkinitema 2027 - Ruto
Eric Buyanza
April 27, 2026
Share :

Rais William Ruto wa Kenya amewaomba wapiga kura wa Mlima Kenya wasimuondoe madarakani katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, badala yake wamuunge mkono kwa muhula wa pili akisema ametekeleza ahadi alizotoa kabla ya uchaguzi wa 2022.
Akizungumza akiwa katika ziara yake ya Kaunti ya Murang’a, Rais Ruto aliwataka wananchi wa eneo hilo kukumbuka mchango wake wa muda mrefu, akisema amekuwa akijihusisha na shughuli za kijamii ikiwemo ujenzi wa makanisa na ziara za mara kwa mara kwa zaidi ya miaka 20, jambo linalomfanya kuwa rafiki wa eneo hilo.
“Niliwajia mwaka 2022, nikawaahidi huduma na ninaendelea kutekeleza. Msisikilize wanaonitukana na kuwachochea dhidi yangu. Mimi ni chaguo lenu bora,” alisema akiwa katika ziara ya siku mbili katika maeneo bunge ya Mathioya, Kiharu na Gatanga.
Alisema anatambua changamoto ndogo zilizojitokeza lakini ataendelea kurejea eneo hilo mara kwa mara ili kuhakikisha umoja unapatikana.
TAIFALEO





