Hali ni tete, mafuriko yaacha watu 10,000 bila makazi
Eric Buyanza
April 10, 2024
Share :
Zaidi ya kaya 2,500 katika Kata ya Muhoro, wilayani Rufiji, mkoani Pwani zimeathiriwa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Imeelezwa kuwa mafuriko hayo yamesababisha zaidi ya wananchi 10,000 kukosa mahali pa kuishi.
Diwani wa Muhoro, Abdul Chobo, akizungumza jana, alisema mafuriko hayo yamewaacha katika hali ngumu kwa kuwa wengi wao hawana mahali pa kushi, huku mali na mashamba yao yakiharibiwa na maji.
Alisema wananchi waliokosa makazi kutokana na mafuriko ni wengi, wakihifadhiwa shuleni na wengine kupata hifadhi kwa ndugu.
"Kuna baadhi ya shule za msingi zimezingirwa na maji. Kwa mfano, Shule ya Msingi Muhoro imefungwa na nyingine wataalamu wanaendelea kufanya tathmini kuona kama zitafungwa au la.
"Kuna watoto wa sekondari wanaohitaji kuvuka maji ili wafike shuleni na kurudi majumbani, lakini wameshindwa kutokana na mafuriko. Wananchi wengi wamepoteza mazao, mashamba na mifugo yao," alisema diwani huyo.
Chobo alisema kuwa awali Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) ilitahadharisha na kuwataka kuchukua hatua za kuhama, lakini wengine walipuuza ingawa kuna wachache waliochukua hatua na wameepuka madhara hayo.
Alisema kutokana na mvua ilivyokuwa inanyesha kwa wingi, walitarajia kupata mafuriko hayo tangu Desemba mwaka jana, lakini kuwapo Mradi wa Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), kumesaidia kuzuia athari zaidi.
Hata hivyo, kuna dhana kwamba kufunguliwa kwa milango ya bwawa hilo kumesababisha hali inayoshuhudiwa sasa Rufiji.
"Hatuwezi kusema bwawa limesababisha mafuriko, si mara ya kwanza kutokea. Mara ya mwisho yalitokea mwaka 2020. Je, kulikuwa na bwawa? Je, na yale yaliyotokea mwaka 1978 na 1998 yalisababishwa na bwawa? Kwahiyo, bwawa si sehemu ni matokeo ya mvua kubwa na asili ya Rufiji," alisema.
Diwani huyo alisema kilio kikubwa kwa sasa ni chakula na makazi mengine ya dharura, ili waliothiriwa wapate mahali pa kujisitiri huku wakisubiri hatua za serikali.
CHANZO: NIPASHE