Hali tete! Trump atishia kufanya mashambulizi makali Iran
Eric Buyanza
July 30, 2026
Share :

Rais wa Marekani, Donald Trump ameonya kuwa nchi yake inaweza kuchukua hatua kali za kijeshi dhidi ya Iran baada ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Washington na Tehran, hali inayozidisha hofu ya kuzuka kwa mapigano mapana zaidi.
Trump ameapa kujibu kwa nguvu kubwa dhidi ya Iran baada ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu kushambulia kambi za kijeshi za Marekani nchini Jordan siku ya Jumatano, huku mvutano wa Mashariki ya Kati ukiongezeka tena na kuyahusisha kwa mara nyingine makundi yanayoungwa mkono na Tehran.
Trump alitoa onyo hilo baada ya kipindi cha utulivu kilichokuwa kimeibua matumaini kwamba Washington na Tehran zingerejea kwenye mazungumzo.
Akizungumza na shirika la habari la Fox News, Trump alisema: "Tutawashambulia kwa nguvu kubwa... Tutawashinda vibaya kabisa."
Kauli hiyo ilisababisha bei za mafuta duniani kupanda kwa asilimia tano kutokana na hofu ya kuvurugika kwa usambazaji wa mafuta katika soko la kimataifa.
Mafuta ghafi aina ya Brent, ambayo ndiyo kipimo kikuu cha bei za kimataifa, yalipanda kwa asilimia 7.3 na kufikia dola 88.09 kwa pipa.
Siku ya Jumatano, Saudi Arabia na Marekani zilitangaza kufanya mashambulizi dhidi ya kambi za wanamgambo wanaoungwa mkono na Tehran nchini Iraq. Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya wapiganaji 20 pamoja na washauri sita wa kijeshi wa Iran.





