Hasheem Thabeet kuirudisha Kikapu kwa vijana
Sisti Herman
March 4, 2026
Share :

Rais mpya wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania, Hasheem Thabeet amesisitiza kuendeleza mpira wa kikapu nchini kwa kuhakikisha ligi inachezwa mikoa yote ya Tanzania, badala ya Dar es Salaam pekee. Thabeet, ambaye ni mchezaji wa zamani wa Ligi ya NBA na sasa anakipiga Dar City, amesema ataleta pia mashindano kama NBA Africa, NBA Academy, BAL na Giants of Africa nchini.
Nyota huyo aliwashukuru viongozi waliopita kwa mchango wao, huku akisisitiza atakuza miradi waliyoiacha. Thabeet pia amesisitiza kuandaa vijana wa timu za taifa mapema kupitia program za kuanzia U-13, U-15, U-18, U-21 na wakubwa ili kukuza vipaji mapema.
Kocha wa Game Time Squad, Bainazi Wamauza, amempongeza Thabeet akisema ana uwezo wa kufanya Tanzania kuwa tishio katika mpira wa kikapu, akilinganisha na Luol Deng, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Sudan Kusini na mchezaji wa zamani wa Chicago Bulls.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Dodoma Hotel, Thabeet alishinda kwa kura 34 dhidi ya mpinzani wake Leonard Benedict aliyepata 25. Mohamed Haruna Kasiji alichaguliwa Makamu wa Rais, huku Mweze Kabida akishinda nafasi ya Katibu Mkuu kwa kura 35 dhidi ya mpinzani wake Robert Manyerere aliyepata 25.
Thabeet amekiri changamoto za ligi za mikoa mbali na Dar es Salaam, lakini anasisitiza kuwa uongozi wake utaleta maendeleo mapya na kuendeleza mpira wa kikapu kwa viwango vya kitaifa na kimataifa. Lengo lake ni kuhakikisha kila mkoa unakuwa na ligi, kuandaa vipaji mapema, na kuongeza mashindano makubwa ya kikapu nchini.





