Hatimae Kongo na M23 kuingia makubaliano
Eric Buyanza
April 25, 2025
Share :
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kundi la waasi la M23 wametoa tamko la pamoja , wakitangaza kuwa wamekubaliana kusitisha mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo.
Hatua hii mpya imefikiwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Qatar, na ni ya kipekee kwa kuwa makubaliano mengi ya awali ya kusitisha mapigano tangu mwaka 2021 yameshindwa kufanikiwa.
Pande zote mbili zimeahidi kufanya kazi pamoja kufikia mkataba wa amani wa kudumu, na wamesema kuwa watatekeleza usitishaji wa mapigano "muda wote wa mazungumzo hadi yatakapokamilika.” Serikali ya Qatar imekaribisha hatua hii, na kutoa wito kwa pande husika kuendelea na juhudi za kuleta amani ya kweli.
Hii ni mara ya kwanza kwa tamko la kusitisha mapigano kutolewa kwa pamoja na serikali ya DRC na M23. Awali, matamko kama haya yalikuwa ya upande mmoja na mara nyingi yalikiukwa ndani ya muda mfupi. Rais wa DRC Félix Tshisekedi alikuwa amekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na M23, akiwashtumu kutumiwa na Rwanda – madai ambayo serikali ya Kigali imekanusha mara kwa mara.