Hatuna chaguo ila kutumia silaha za nyuklia - Iran
Eric Buyanza
April 1, 2025
Share :
Iran imesema haitakuwa na njia nyingine ila kutumia silaha za nyuklia endapo itashambuliwa na Marekani au washirika wake. Hayo ni kufutia kitisho cha rais wa Marekani Donald Trump aliyesema ataishambulia Iran kijeshi.
Ali Larijani, Mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, amesema kwenye mahojiano na televisheni ya taifa la Iran kwamba "hawaelekei kwenye kuunda silaha za nyuklia, lakini ikiwa Marekani itafanya makosa katika swala hilo basi Iran italazimika kuelekea kwenye mkondo huo kwa sababu inapaswa kujilinda."
Kauli hii ameitoa saa chache baada ya kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei, kuahidi kuijibu Marekani endapo Trump atatimiza tishio lake la kulishambulia taifa hilo la Kiislamu.
Larijani amesisitiza kauli hiyo ya Kiongozi Mkuu kwamba Iran italazimika kuchukua hatua tofauti iwapo Marekani itaishambulia nchi yake kwa mabomu au kupitia kwa Israel.
"Tumesema kuna amri ya kidini inayokataza kutengeneza silaha za nyuklia, tunatoa ushirikiano kwa shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia (IAEA) na hivyo hatupangi kujielekeza kwenye silaha ya nyuklia, lakini Marekani ikifanya makosa kuhusiana na suala la nyuklia la Iran, itatulazimisha kufuata njia hiyo, kwa sababu Iran inapaswa kujilinda.".
DW