Hii ndio mipango ya Benchikah kwa Wydad
Eric Buyanza
December 9, 2023
Share :
Ukiwa mchezo wa pili kwa kocha mkuu Abdelhak Benchikah ugenini, leo Simba Sc watakuwa dimbani dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco kwenye mechi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha huyo na mastaa wa timu hiyo wakiwatoa hofu mashabiki.
"Lengo kubwa ni alama tatu, nawafahamu wapinzani wetu si mara ya kwanza kukutana nao, wana timu nzuri ila na imani tutakuwa bora zaidi yao" alisema Benchika alipokuwa kwenye mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo.
"Hii ni mechi muhimu kwetu kupata alama ugenini ili kutengeneza mazingira mazuri ya kufuzu robo fainali, tukipata alama hapa itatuongezea kujiamini na kupata alama zingine kwenye mchezo wa marudiano dhidi yao nyumbani wiki ijayo" alimaliza Fabrice Ngoma kwa niaba ya wachezaji wenzake kwenye mkutano na waandishi wa habari kabla ya mchezo huo.
Simba itashuka kwenye Uwanja wa Marrakech, Morocco katika pambano la Kundi B ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare mbili mfululizo za mechi za awali, lakini mastaa wa Simba wameapa kushinda mechi ya leo ili kujiweka pazuri na kuwarudishia furaha mashabiki wa timu hiyo.
Simba imepania kurudia kile kilichofanywa na Jwaneng Galaxy wiki mbili zilizopita kwa kuibuka na ushindi ugenini dhidi ya Wydad wakati wakiwashukia wenyeji wao hao kuanzia saa 4:00 usiku.