Hizi hapa Hospitali zinazotoa huduma ya 'Tiba Asilia'
Eric Buyanza
May 17, 2025
Share :
Kama unasumbuliwa na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza na unahitaji tiba za dawa za asili, Serikali imetaja hospitali 14 za mikoa ambazo tiba hizo hutolewa, ogopa matapeli.
Hospitali hizo zimeongezeka kutoka saba ambazo Serikali, mwaka 2023, ilizitangaza kuanza kutoa huduma hiyo, sasa zimefika 14.
Daktari humpima mgonjwa na kumweleza tatizo lake na aina ya dawa zinazotibu tatizo lake ili kupata huduma ya tiba asilia katika hospitali hizo, naye huchagua ama kutumia tiba asilia au tiba ya kisasa.
Awali, hospitali saba ambazo zilianza kutoa matibabu jumuishi ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Morogoro, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Mwanza Sekou-Toure, Arusha Mount Meru, Tanga Bombo na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya.
Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya, Dk Mussa Lipukuta amebainisha ongezeko la hospitali hizo wakati wa mkutano uliowakutanisha wataalamu wa tiba asili, waganga wafawidhi wa mikoa na wafamasia waliokutana kujadili namna ya kuboresha utoaji huduma za tiba asili ndani ya hospitali.
MWANANCHI