Hizi ndizo 'Dabi 6' zisizosahaulika na wapenzi wa soka
Eric Buyanza
April 20, 2024
Share :
Hizi ndizo baadhi ya mechi za Simba na Yanga zilizoacha simulizi miongoni mwa wapenzi wa soka hapa Tanzania
1. Yanga 5-0 Simba (1968)
Mechi hii imeingia katika rekodi ya kuwa ni ya kwanza timu hizo kufungana mabao mengi katika mechi za dabi. Hii ilikuwa ni Juni Mosi, mwaka 1968. Yanga ikiiadhibu Simba mabao 5-0, ambayo yalifungwa na Maulidi Dilunga (mawili), Kitwana Manara (mawili) na Salehe Zimbwe alifunga bao moja.
2. Simba 6-0 Yanga (1977)
Simba ililipa kisasi cha kufungwa mabao 5-0 miaka tisa baadaye, ilipoikandika Yanga magoli 6-0, mechi ambayo hadi leo inashika rekodi ya timu kufungwa mabao mengi zaidi katika dabi.
Ni mechi ambayo pia imeweka rekodi ambao haijavunjwa kwa mshambuliaji wake, Abdallah Kibadeni 'King' kufunga hat-trick'.
Mechi ilichezwa Julai 19, mwaka 1977, na mbali na King Kibadeni, mabao mengine mawili yalifungwa na Jumanne Hassan 'Masimanti' na beki, Selemani Sanga wa Yanga akijifunga mwenyewe.
3. Simba 4-4 Yanga (1996)
Mechi hii inabaki katika vitabu vya kumbukumbu kuwa ndiyo sare iliyozaa mabao mengi zaidi kwenye mchezo wa dabi.
Mechi ilichezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini, Arusha, mabao ya Yanga yakifungwa na Edibily Lunyamila, Mustapha Hozza (akijifunga), Said Mwamba 'Kizota' na Sanifu Lazaro, huku ya Simba yakipachikwa na Thomas Kipese, Ahmed Mwinyimkuu na Dua Said akipiga mawili.
4. Simba 5-0 Yanga (2011/12)
Ni moja kati ya mechi za kukumbukwa za watani wa jadi, ikichezwa Mei 6, mwaka 2012, Simba ilipata matokeo hayo kupitia mabao yaliyowekwa kimiani na Emmanuel Okwi, aliyefunga mawili, Felix Sunzu, Patrick Mafisango (marehemu) na Juma Kaseja, wote wakifunga magoli hayo kwa penalti.
5. Simba 3-3 Yanga (2013/14)
Ilikuwa ni moja kati ya dabi za kushangaza ambapo hadi mapumziko Yanga ilikuwa ikiongoza mabao 3-0, lakini Simba ikarudisha magoli yote kipindi cha pili.
Dabi hiyo ilichezwa Oktoba 20, mwaka 2013, Yanga ikitangulia kwa mabao ya Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza wakati Simba ilisawazisha kupitia Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
6. Yanga 5-1 Simba (2023/24)
Hii ni dabi ya mzunguko wa kwanza msimu huu, ambapo Yanga ilitoa kipigo kikubwa cha mabao 5-1, mechi iliyochezwa Novemba 5, mwaka jana.
Yalikuwa ni mabao ya Kennedy Musonda, Maxi Nzengeli (mawili), Stephane Aziz Ki na Pacome Zouzoua.