Ibada yasimama baada ya jamaa kujaribu kumpiga risasi mchungaji
Eric Buyanza
May 6, 2024
Share :
Huko Pennsylvania nchini Marekani ibada ilisitishwa ghafla siku Jumapili, Mei 5, baada ya mwanaume mmoja kuingia kwenye kanisa la (Jesus Dwelling Place) na kwenda moja kwa moja mbele ya kanisa akiwa amemnyooshea bunduki mchungaji wa kanisa hilo akitaka kumpiga risasi, hata hivyo kwa hali ya kushangaza bunduki hiyo iligoma kufyatuka.
Mwanaume huyo ambaye polisi walimtaja kwa jina la Bernard Junior mwenye umri wa miaka 26, baada ya bunduki yake kugoma kufyafuta ndipo waumini wakishirikiana na mchungaji huyo walipofanikiwa kumkamata na kumnyang'anya silaha kabla haijasababisha madhara.
"Ninamshukuru Mungu kwamba bado niko hapa kwa sababu kwa hakika alinisaidia," Mchungaji Glenn aliliambia shirika la habari la ABC News.
Akielezea tukio hilo la kutisha, Mchungaji huyo alisema; "Nilianza kuhubiri, na ghafla, kutoka upande wangu wa kushoto, nilimwona akisogea kutoka nyuma kwenda mbele ya kanisa, na akaketi kwenye kona ya mbele ya kanisa huku akitabasamu," ilisema. "Ghafla, niliona tu bunduki ikinielekea moja kwa moja.
Na wakati huo, nilichoweza kujaribu kufanya ni kukimbia ili kujificha," alisema.
Mtu huyo alishikiliwa kanisani hapo hadi Polisi walipofika eneo la tukio na kumkamata.