IJUE: (Al Nahyan) familia tajiri zaidi duniani
Eric Buyanza
March 13, 2024
Share :
Familia ya kifalme ya Abu Dhabi, Al Nahyan, ndiyo iliyoongoza orodha ya familia tajiri zaidi duniani mwaka huu ikiwa na utajiri wa dola bilioni 305, ikiipiku familia ya Walton ya Marekani, wamiliki wa maduka ya Walmart kwa kiasi cha dola bilioni 45.
Familia ya Al Nahyan inadhibiti eneo lenye utajiri wa mafuta ghafi la UAE la Abu Dhabi na inamiliki Manchester City, klabu maarufu zaidi ya kandanda duniani.
HISTORIA YA FAMILIA YA AL NAHYAN
Abu Dhabi, mojawapo ya majimbo saba ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mji mkuu wa nchi hiyo na ina akiba nyingi ya mafuta.
Familia hiyo ilitawala eneo hilo kwa miongo kadhaa kabla ya kugunduliwa mafuta. Lakini wakati huo haikuwa tajiri kama ilivyo sasa.
Hadithi ya Falme za Kiarabu na familia ya Al Nahyan ilianza katika miaka ya 1960 na ugunduzi wa mafuta katika eneo hilo.
Hapo awali, idadi kubwa ya wakazi wa nchi hiyo walikosa huduma za kimsingi, lakini mara baada ya kupatikana mafuta, Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan alilibadilisha eneo hilo na kuziunganisha falme zote za eneo hilo na kuunda nchi inayoitwa Umoja wa Falme za Kiarabu.
Sheikh Zayed bin Sultan Al Nahyan pia anaitwa 'Baba wa Taifa' na alifanywa kuwa Rais wa nchi mwaka 1971.
Mwaka wa 2004 mwanawe Sheikh Khalifa bin Zayed Al Nahyan alimrithi baba yake kama mkuu wa UAE. Mwaka 2022 Sheikh Mohammed bin Zayed Al Nahyan, aliyesoma katika Chuo cha Kijeshi cha Uingereza huko Sandhurst, akawa Rais wa tatu wa UAE.
Wengine katika familia ya Al Nahyan hutekeleza majukumu katika serikali ya UAE na sekta binafsi.
Burj Khalifa, jengo refu zaidi duniani huko Dubai, limepewa jina kwa heshima ya Rais wa zamani wa UAE, Khalifa bin Zayed Al Nahyan.