Ikiwa Bunge litaidhinisha, Itakuwa nchi ya kwanza Duniani kuruhusu Ukeketaji
Eric Buyanza
April 20, 2024
Share :
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa wito kwa wabunge wa nchini Gambia kuupinga muswaada wa kutaka kubatilishwa kwa sheria ya kupiga marufuku ukeketaji wa wanawake na wasichana nchini humo.
Shirika hilo la kimataifa limesema muswada huo unasababisha mashaka makubwa katika suala la haki za wanawake.
Ukeketaji ni kitendo kilichopigwa marufuku kisheria katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi tangu mwaka 2015, lakini mwezi March mwaka huu wabunge walipiga kura ya kuupeleka muswaada huo wenye utata kwenye kamati maalum ya kuutathmini kabla ya bunge kuchukua hatua ya mwisho ya kuupigia kura.
Shirika la Human Rights Watch limesema, ikiwa bunge litaidhinisha muswaada huo basi Gambia itakuwa nchi ya kwanza duniani kuruhusu tena ukeketaji.
Itakumbukwa Jumatatu ya Machi 18, 2024 wabunge wa Gambia walitaka kuondolewa kwa marufuku ya ukeketaji nchini humo.
Mbunge aliyewasilisha muswada huo alitumia hoja za kidini na kimila.
Kulingana na mbunge huyo kupiga marufuku tabia hii kunakiuka haki ya watu wa Gambia kutekeleza utamaduni wao na mila iliyokita mizizi.