Injinia soma hiyo....! Mwenye shughuli zake anarejea mzigoni.
Joyce Shedrack
July 21, 2024
Share :
Siku ya leo Julai 21 aliyekuwa msemaji wa klabu ya Yanga Haji Sunday Manara anatimiza miaka miwili tangu alipofungiwa kutojihusisha na mchezo wa mpira wa miguu mwaka 2022 baada ya kukutwa na hatia ya kutoa baadhi ya matamshi ambayo yaliashiria kumdhalilisha Rais wa TFF Wallace Karia.
Julai 21 mwaka 2022 Kamati ya Maadili ya TFF ilitangaza kutoa hukumu hiyo ya kifungo cha miaka miwili kutojihusisha na masuala ya soka pamoja na faini ya shilingi milioni 20.
Shauri hilo namba 2 la kesi ya maadili lilifunguliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF dhidi ya Msemaji wa Yanga Haji Manara na Kamati ya maadili ya TFF ikakutana kwa mara ya kwanza Julai 11, 2022 kusikiliza shauri hilo.
Wakati ikitoa taarifa ya hukumu hiyo mbele ya waandishi wa habari kamati hiyo ilibainisha kuwa adhabu hiyo inaanza siku hiyo hiyo ya Julai 21, 2022.
Kwa mantiki hiyo adhabu ya kufungiwa miaka miwili kwa msemaji huyo inatamatika leo julai 21,2024 ikiwa ni baada ya kutimiza miaka miwili tangu hukumu hiyo itolewe.
Huwenda tukamshuhudia Msemaji huyo maarufu siku ya kilele cha wananchi Yanga Day akijitokeza uwanjani kwa mara ya kwanza tangu akumbane na adhabu hiyo.