Iran kutoa milioni 79 kwa atakayeua au kumkamata mwanajeshi wa Marekani
Eric Buyanza
August 17, 2026
Share :

Kamanda wa Jeshi la Iran, Amir Hatami, ametangaza kuwa yeyote atakayemuua au kumkamata mwanajeshi wa Marekani na kumkabidhi kwa mamlaka atapewa zawadi ya dola 30,000; lakini ikiwa mwanamke atafanya hivyo, zawadi hiyo itaongezwa maradufu.
Kulingana na ripoti ya shirika la habari la serikali ya Iran (IRNA), Hatami alisema uamuzi huo umefikiwa kufuatia maombi mengi kutoka kwa wananchi waliotaka kuchangia fedha za zawadi hiyo.
"Jeshi litatoa zawadi ya dola 30,000 kwa yeyote atakayemuua au kumkamata afis wa vikosi vya Marekani, na ikiwa mwanamke atafanya hivyo, zawadi hiyo itaongezwa maradufu," IRNA ilimnukuu Hatami akisema.
Hakutaja muda au mahali maalum ambapo mashambulizi hayo yanayoweza kutokea.
Hakuna ripoti rasmi iliyotolewa kuhusu uwepo wa vikosi vya ardhini vya Marekani ndani ya Iran tangu kuanza kwa vita, isipokuwa tukio moja la mwezi Aprili mwaka jana la kuokelewa rubani wa ndege ya Marekani iliyoanguka.
Kamanda huyo wa jeshi la Iran aliongeza kusema, "Uwepo wa Marekani kimsingi 'umeshafukuzwa' kutoka eneo hili na kwa mtazamo wa Tehran, vikosi vya Marekani havina tena haki ya kuingia katika Ghuba, Lango la Hormuz, na Bahari ya Oman."





