Iran yasema makubaliano sio ushindi kwa Marekani
Eric Buyanza
June 25, 2026
Share :
Mkuu wa timu ya upatanishi ya Iran, Mohammad Bagher Qalibaf, ameyataja makubaliano yanayoendelea sasa kati ya nchi yake na Marekani kuwa ni "tangazo la kushindwa la Washington".
Akizungumza kupitia idhaa ya Kiazeri kwenye televisheni ya Iran siku ya Jumatano (Juni 24), Qalibaf alisema Makubaliano ya Islamabad hayakutokana na shinikizo na vitisho "bali yalikuwa matokeo ya mapambano na mamlaka ya taifa jasiri la Iran."
"Ndio maana Makubaliano hayo yamekuwa tangazo la Marekani kushindwa vita." Aliongeza.
Qalibaf, Spika wa Bunge na mwanasiasa mwenye ushawishi na uzoefu mkubwa wa masuala ya kijeshi na kiutawala, alizungumza hayo akiwa ndio kwanza amerejea akitokea nchini Oman, alikokwenda kuzungumzia hatima ya Mlango Bahari wa Hormuz na taifa hilo jirani, ambalo kwa pamoja na Iran, wanaumiliki ujia huo muhimu kwa kupitishia nishati ya mafuta na gesi ulimwenguni.
Alisema kuanzia sasa ni jukumu la mataifa ya Mashariki ya Kati na Ghuba pekee kuhakikisha usalama wa eneo lao na sio la mgeni yeyote, akimaanisha Marekani na washirika wake wa Magharibi, bila kuwataja kwa majina.
DW






