Iran yashambulia vituo 85 vya jeshi la Marekani
Eric Buyanza
July 8, 2026
Share :


Jeshi la Iran limetangaza kuwa limeanzisha mashambulizi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Marekani katika kile lilichokitaja kuwa ni jibu la mashambulizi yaliyofanywa na Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) dhidi ya zaidi ya malengo 80 kusini mwa Iran.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatano, Julai 8, IRGC ilidai kuwa Marekani ilikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na makubaliano ya Islamabad kwa kufanya mashambulizi ya anga mapema asubuhi dhidi ya vituo vya pwani na maeneo ya kiraia katika mikoa ya Hormozgan na Mahshahr.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, katika "hatua ya awali ya kujibu uchokozi huo," vikosi vya majini na anga vya IRGC vilifanya mashambulizi ya pamoja ya makombora na ndege zisizo na rubani (droni), yakidai kulenga na kuharibu vituo 85 muhimu vya kijeshi vya Marekani, vikiwemo eneo la Port Salman, Makao Makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani nchini Bahrain, pamoja na Kambi ya Anga ya Ali Salem nchini Kuwait.
IRGC pia ilidai kuwa ilidungua ndege moja isiyo na rubani aina ya MQ-9 ya Marekani iliyokuwa ikijaribu kuingilia operesheni hiyo.
Kabla ya tangazo hilo, jeshi la Kuwait lilisema lilikuwa limewasha mifumo yake ya ulinzi kutokana na kile lilichokiita mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani, huku pia kukiwa na ripoti za ving'ora vya tahadhari kusikika nchini Bahrain.
Tangazo la IRGC kuhusu mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi ya Marekani nchini Kuwait na Bahrain limetolewa wakati Iran imeendelea kukanusha kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli tatu za kubeba mafuta katika Mlango wa Hormuz yaliyotokea Jumanne, Julai 6.
Mashambulizi hayo yamezua mzozo mpya wa kijeshi kati ya Iran na Marekani. Wakati Iran ikikanusha kuhusika, Qatar, Saudi Arabia na Marekani zimeilaumu IRGC kwa kuhusika na mashambulizi dhidi ya meli hizo.





