Ismail Elfath ndiye mwamuzi wa mechi ya Argentina na England
Eric Buyanza
July 14, 2026
Share :

Waamuzi watakaosimamia mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia kati ya England na Argentina wametangazwa rasmi, huku mwamuzi Ismail Elfath akipewa jukumu la kuongoza pambano hilo kubwa.
Elfath, ambaye alikuwa mwamuzi wa nne katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2022, atakuwa mwamuzi mkuu wa mechi hiyo itakayopigwa jijini Atlanta.
Mwamuzi huyo ana uzoefu mkubwa katika mashindano ya kimataifa na si mgeni kwa kikosi cha Argentina kinachoongozwa na Lionel Messi, baada ya kuwahi kusimamia mechi kadhaa zilizowahusisha mabingwa hao wa dunia.
Mwamuzi Ismail Elfath, ambaye alizaliwa nchini Morocco lakini akalelewa nchini Marekani, alikuwa mwamuzi wa nne katika fainali ya Kombe la Dunia 2022 iliyowakutanisha Argentina na Ufaransa, na Argentina kushinda kwa mikwaju ya penati 4-2, kufuatia sare ya mabao 3-3 ndani ya dakika 120 za mchezo.
Macho ya mashabiki wa soka duniani yatakuwa kwa waamuzi wa mchezo huo wa Jumatano kufuatia madai yaliyoibuka kutoka kwa baadhi ya wadau kwamba mashindano hayo yanapangwa kwa lengo la kuhakikisha mabingwa watetezi, Argentina, wanafuzu kucheza fainali.
Katika mchezo huo, Ismail Elfath atasaidiwa na waamuzi wasaidizi kutoka Marekani, Corey Parker na Kyle Atkins.
Aidha, waamuzi kutoka Italia, Maurizio Mariani na Daniele Bindoni, watakuwa sehemu ya jopo hilo, huku Mariani akiteuliwa kuwa mwamuzi wa nne na Bindoni akiwa mwamuzi msaidizi wa akiba.





