Israel kupunguza maelfu ya wanajeshi wake Gaza
Eric Buyanza
January 2, 2024
Share :
Jeshi la Israel limetangaza kuwa litawaondoa maelfu ya wanajeshi wake kutoka Ukanda wa Gaza uliozingirwa katika hatua ya kwanza muhimu ya kurudisha nyuma wanajeshi wake tangu kuanza kwa vita hivyo Oktoba mwaka jana.
Hata hivyo jeshi hilo limezidisha mashambulizi yake huko Gaza licha ya tangazo la kupunguza maelfu ya wanajeshi wake katika ukanda huo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, likimnukuu afisa wa Israel aliyesema siku ya Jumatatu kuwa wanajeshi wataondolewa ndani ya Gaza mwezi huu na kuingia kwenye awamu nyingine ya operesheni hiyo.
Afisa huyo amesema kupunguzwa kwa wanajeshi kutawaruhusu baadhi ya askari wa akiba kurejea katika maisha ya kiraia, kuinua uchumi wa Israel ulioathiriwa na vita na kuwaweka tayari wanajeshi iwapo mzozo wa kaskazini mwa Lebanon na Hezbollah utaongezeka.
Afisa mmoja wa Marekani amekaririwa akisema uamuzi huo wa Israel unaashiria kuanza kwa mabadiliko ya operesheni za Israel.
Marekani imekuwa ikiitaka Israel kupunguza makali ya operesheni yake ya kijeshi, huku kukiwa na wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano wakati idadi ya vifo ikiongezeka.