Israel yaamuru raia 100,000 kuondoka Rafah
Eric Buyanza
May 6, 2024
Share :
Jeshi la Israel limewaamuru maelfu ya watu kuondoka katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah, hii ikiashiria kuwa operesheni ya kijeshi iliyokuwa ikitajwa kwa muda mrefu huenda ikawa inakaribia kuanza.
Tangazo hilo la Israel limekwamisha juhudi za hivi karibuni za wapatanishi wa kimataifa, ikiwa ni pamoja na Marekani, Qatar na Misri za kutafuta kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza .
Viongozi wa Kundi la Hamas pamoja na maafisa wa Qatar ambao ndiyo wapatanishi wakuu, wameonya kuwa uvamizi wa Rafah unaweza kuharibu mchakato wa mazungumzo ya kusaka makubaliano ya usitishwaji mapigano.
Mazungumzo hayo yaliyondelea hadi usiku wa jana mjini Cairo yameshindwa kufikia muafaka kutokana na misimamo ya pande zote.
Hamas imesema kamwe haitoafiki makubaliano yoyote ambayo hayatohusisha usitishwaji kamili wa vita na kuondoka kabisa kwa vikosi vya Israel katika ardhi ya Palestina, jambo ambalo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema hawawezi kamwe kukubaliana nalo.
DW