Issa mbaroni kwa kumbaka na kumpa mimba mtoto wake
Eric Buyanza
July 29, 2024
Share :
Mahakama ya Wilaya ya Momba mkoani Songwe imemfikisha mahakamani Issa Mgode (44), mkazi wa Kijiji cha Kokoto, Kata ya Mpemba, Wilaya ya Momba kujibu shtaka la kumbaka na kumpa ujauzito mtoto wake wa kufikia mwenye umri wa miaka (13) (jina limehifadhiwa).
Mkuu wa Mashtaka Wilaya ya Momba, Simon Peres alisema mtuhumiwa amefunguliwa kesi namba 20886/2024 baada ya mahakama hiyo kusikiliza ushahidi upande wa Jamhuri na utetezi upande wa mshtakiwa.
Mshtakiwa huyo alisomewa shitaka kwa kosa hilo alilofanya kinyume cha Sheria chini ya Kifungu cha Sheria cha 130 (1) na (2)(e) na kifungu cha 131 (3) Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16.
Alisema mshtakiwa aligundulika kufanya kosa hilo Juni 29, mwaka huu baada ya mtoto wake wa kufikia aliyekuwa akimlea kutokana na kumuoa mama yake kugundulika ana ujauzito baada ya kupimwa afya na mama yake aliyefanya uamuzi huo baada ya mabadiliko ya kimwili kwa mtoto huyo.
Peres alisema mtoto huyo aliieleza mahakama kuwa baba yake wa kambo alianza kumbaka tangu Aprili, 2024 baada ya mama yake kuondoka siku kadhaa kwenda kuvuna maharage katika Kijiji cha Ikomela wilayani Mbozi.
Alisema alimfanyia ukatili huo huku akimtishia kumpiga ikiwa atasema kwa majirani au kwa mama yake mzazi atakaporudi nyumbani kutoka shambani.
“Kwa maelezo ya mtoto, baba yake huyo mlezi tangu Aprili, 2024 aliendelea kumfanyia ukatili huo wa kumbaka mara kwa mara, ambapo mara ya mwisho ilikuwa Juni katikati mwaka huu,” alisema mkuu wa mashtaka.
Hakimu wa kesi hiyo, Tagha Komba ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi Wilaya ya Momba alisema baada ya mahakama kusikiliza pande zote mbili upande wa Jamhuri na upande wa mshtakiwa, kesi hiyo itasikilizwa tena Agosti Mosi, 2024.
TSN