Itachukua miaka 16 kuijenga upya Gaza - UN
Eric Buyanza
May 3, 2024
Share :
Umoja wa Mataifa unakisia kwamba itagharimu hadi dola bilioni 40 na miaka 16 kuweza kuurejesha Ukanda wa Gaza kwenye hali ya kawaida baada ya uharibifu mkubwa kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu Vita vya Pili vya Dunia.
Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Abdallah al-Dardari, amesema makisio ya awali ya Mfuko Maendeleo wa Umoja huo yalikuwa yanaonesha kwamba ujezi mpya wa Gaza utatumia dola bilioni 30 na kwamba unaweza kufikia hadi dola bilioni 40.
"Kiwango cha uharibifu ni kikubwa mno na kisichokadirika. Hii ni hali ambayo jamii ya kilimwengu haijawahi kukabiliana nayo tangu Vita vya Pili vya Dunia." alisema Dardari.
Umoja wa Mataifa unakisia kuwa hata kama vita kwenye Ukanda wa Gaza vitamalizika leo, basi itachukuwa miaka 16 kutoka sasa kuweza kuyajenga tena majengo yote yaliyoharibiwa.
Kauli ya msaidizi huyo wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa inaashiria hali halisi ya madhara ambayo yameikumba Gaza tangu Israel ilipoanzisha operesheni yake ya kijeshi kufuatia mashambulizi ya wanamgambo wa Kipalestina ya tarehe 7 Oktoba, ambapo walilivamia eneo la kusini mwa Israel na kusababisha vifo vya watu wapatao 1,200 na kuwachukuwa mateka wengine wapatao 250.
Tangu hapo, Israel imekuwa ikitumia silaha nzito nzito kuteketeza majengo ya aina mbalimbali ndani ya Ukanda wa Gaza, yakiwemo makazi ya watu, hospitali, shule, masoko, misikiti na makanisa.
DW