Je Wajua mwanamke anaweza kupata mimba akiwa na mimba?
Eric Buyanza
July 1, 2026
Share :

Ni jambo linalowezekana kibaiolojia lakini ni nadra sana kutokea kwa binadamu, na kitaalamu hali hii inaitwa 'Superfetation'. Mpaka sasa kuna kesi kama 14 zilizoripotiwa duniani kote.
Kawaida, mwanamke anapopata ujauzito, mwili wake hufunga mifumo yote ya uzazi ili kulinda mimba iliyopo. Hata hivyo, ili 'Superfetation' itokee,
vizuizi vitatu vikuu vya asili vya mwili lazima vifeli kwa wakati mmoja:
JINSI INAVYOTOKEA (VIZUIZI VINAVYOFELI)
1. Ovari Kuendelea Kutoa Yai (Ovulation):
Kawaida, mtu akipata mimba, homoni za estrogen na progesterone huzuia ovari kutoa yai lingine. Kwenye superfetation, ovari hutoa yai lingine la pili wiki chache baada ya mimba ya kwanza kutungwa.
2. Manii Kupenya Kizazi Kilichofungwa:
Baada ya mimba ya kwanza, ute wa mlango wa uzazi (cervical mucus) unakuwa mzito sana na kutengeneza (mucus plug) ili kuzuia manii au bakteria kuingia. Katika hali hii ya kipekee, cervical mucus hushindwa kuzuia, na manii hupenya hadi kwenye mirija ya uzazi.
3. Yai la Pili Kujipandikiza Kwenye Uterus:
Uterus (mji wa mimba) tayari inakuwa imebadilika kwa ajili ya kulea kiinitete cha kwanza, jambo linalofanya iwe vigumu kwa yai lingine kujipandikiza. Hapa, yai la pili lililorutubishwa linafanikiwa kupata nafasi na kujishikiza kwenye ukuta wa uzazi.
BAADHI YA VISA HIVYO
1. Kisa cha Rebecca Roberts (Uingereza, 2020)
Rebecca alikuwa ametumia dawa za kusaidia uzazi (fertility drugs) baada ya kuhangaika kupata mtoto kwa muda mrefu. Kwenye ultrasound ya kwanza ya wiki ya 7 na ya 10, madaktari waliona mtoto mmoja tu (Noah), aliporudi kwenye ultrasound ya wiki ya 21, madaktari walishangaa kuona mtoto wa pili (Rosalie) ambaye hakuwepo mwanzo. Uchambuzi wa kitabibu ulionyesha kuwa Rosalie alitungwa wiki 3 baada ya kaka yake (Noah).
2. Kisa cha Sandra Searle (Australia, 2023)
Sandra alipata ujauzito wa watoto ambao walionekana kama mapacha (Poppy na Michael) lakini walikuwa na utofauti mkubwa wa makuzi. Baada ya vipimo vya kina vya madaktari, iligundulika kuwa watoto hao walitungwa katika nyakati mbili tofauti zenye utofauti wa siku 18.





