pmbet

JE WAJUA: Soko la Kariakoo kilikuwa kituo cha jeshi?

Eric Buyanza

July 1, 2024
Share :

Historia ya jina la Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia tangu enzi za ukoloni wa Mjerumani wakati Tanzania Bara ikiitwa Tanganyika.

Mahala lilipo soko hilo palijengwa jengo la utawala wa Wajerumani ambalo lilikusudiwa litumike kama ukumbi wa kuadhimisha sherehe za kutawazwa kwa Mfalme Kaiser Wilheim wa Ujerumani kwa wakati huo.

Hata hivyo baada ya jengo kukamilika halikutumika kama ilivyokusudiwa kuwa na badala yake lilitumika kama kambi ya kikosi cha wapagazi waliobeba mizigo ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia waliojulikana kama Carrier Corps.

Jina hilo la maaskari wabeba mizigo katika Kiswahili lilitamkwa ‘karia- koo’ na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka jengo hili la Soko la Kariakoo.

Meneja Mkuu wa Soko la Kariakoo, Florens Seiya anasema baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kuisha rasmi mwaka 1919 na nchi Tanganyika kuanza kutawaliwa na Waingereza, jengo hilo lilianza kutumika kama soko na kuhudumia wakazi wa Dar es Salaam.

Anasema wakati huo wafanyabiashara walikuwa wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakuwa na meza. Wafanyabiashara hao waliendelea kufanya biashara zao sakafuni hadi miaka ya 1960, meza za saruji zilipojengwa. Seiya anasema kwa kadiri jiji la Dar es Salaam lilivyokua na wakazi wake kuongezeka, ndivyo soko hilo la lilivyozidiwa na kushindwa kumudu kutoa huduma nzuri kwa wananchi.

Wafanyabiashara walifanya shughuli zao katika hali ngumu kwa sababu kulikuwa na msongamano mkubwa wa watu pia hapakuwepo ghala za kuhifadhia bidhaa.

Hali hiyo iliwafanya viongozi wa halmashauri ya jiji kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya jiji, na hivyo wakaanza kujadili uwezekano wa kujenga soko jipya kubwa na la kisasa. Uamuzi wa kujenga Soko Kuu la Kariakoo ulifanywa na serikali mwaka 1970 ambapo Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam iliagizwa kujenga soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani.

(Na Benjamin Sawe)

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet